Wema Sepetu Miss tz 2006 Kizimbani




MISS Tanzania wa mwaka 2006, Wema Sepetu na mwenzake, Asha Jumbe, wakazi wa Tabata Senene jijini Dar es Salaam, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni wakikabiliwa na tuhuma ya kuharibu mali.

Akisoma hati ya shtaka hilo, Mwendesha Mashtaka Inspekta wa Polisi, Nassoro Sisiwahy mbele ya Hakimu Mfawidhi Emillius Mchauru alisema kuwa watuhumiwa hao walitenda kosa hilo Januari 29 majira ya saa 3:00 usiku maeneo ya Magomeni Mikumi, Dar es Salaam.

Nassoro alidai kuwa siku ya tukio hilo watuhumiwa hao waliharibu kioo cha mbele cha gari aina ya Toyota Rav 4 yenye namba ya usajili T.993 ASD.

Mwendesha mashtaka alidai kuwa kioo cha gari kina thamani ya Sh 1,000,000 mali ya Stephen Kanumba.

Hata hivyo, watuhumiwa hao walikana shtaka hilo na walipelekwa rumande kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ya Sh 500,000, wadhamini wawili, mmoja awe mtumishi wa serikalini.

Awali, mtuhumiwa wa kwanza alikuwa ana mdhamini, lakini cha kushangaza alipofika mahakamani hapo alidai kuwa alikuwa amesahau barua zake kwenye gari.

"Mheshimiwa hakimu naomba nikachukue barua za kumdhamini kwani nimezisahau kwenye gari nilipoitwa mimi nikaja bila kuzichukua, "alisema mdhamini wa mtuhumiwa wa kwanza

Baada ya muda kupita hakimu Mchauru alisema, "Yaani mahakama imsubiri mtu aenda nyumbani kuchukua barua za kumdhamini mtu, kesi hii naiahirisha hadi hapo itakapotajwa tena Machi 18".

No comments: