Bodi ya Tanesco inasubiri nini kujiuzulu?


Bodi ya Tanesco inasubiri nini kujiuzulu?

Ni jambo la kufedhehesha kwamba eti Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco), Dk. Idirs Rashid, amekiuka maagizo ya Bodi ya Wakurugenzi ya shirika hilo juu ya mitambo ya kufua umeme ya Dowans.

Kwamba bodi ikiwa na akili timamu kabisa iliagiza menejimenti ya shirika hilo kwamba iachane na mitambo ya Dowans, lakini Dk. Rashid akapuuza maelekezo hayo na kwenda kwenye Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma na kuwasilisha kilio cha kutaka kuinunua kutokana na kilichoelezwa uhaba wa umeme utakaokabili taifa baadaye mwaka huu.

Baada ya Dk. Rashid kuwasilisha hoja yake kwa Kamati hiyo, amekutana na upinzani mkali kutoka kwa wadau mbalimbali juu ya nia ya Tanesco ya kununua mitambo hiyo.

Lakini zaidi kauli ya bosi huyo aliyotoa mbele ya waandishi wa habari wakati akitangaza kwamba wameondoa nia yao ya kuwania kununua mitambo hiyo, nayo imeudhi watu wengi kutokana na kutishia wananchi kwamba taifa litaingia gizani na wasilaumiwe.

Kwa ujumla suala la mitambo ya Dowans limefunikwa na sintajua nyingi, ukiukaji wa taratibu na upuuzaji wa maelekezo kwa upande wa watendaji wa Tanesco kiasi cha kuamsha maswali mengi na magumu juu ya sababu ya hali hiyo kutokea.

Yapo maelezo mengi yametolewa juu ya mitambo ya Dowans wapo wanaosema kwamba mitambo hii ni muhimu kwa ajili ya kufanikisha mikakati ya Tanesco kujipanga kukabiliana na uhaba wa maji katika mabwawa pia wapo wanaosema kwamba mitambo hiyo ikinunuliwa itapunguza adha na mchakato mrefu wa kuanza kuagiza mitambo mipya.

Pamoja na misimamo ya hoja hizo hapo juu, wapo wanaosema kwamba mitambo ya Dowans ni haramu kutokana na kuwa na mahusiano na mkataba wa kampuni ya Richmond Development Corporation iliyoingia mkataba wa kilaghai na Tanesco mwaka 2006.

Kwa kuzingatia hali hiyo pamoja na azimio la Bunge juu ya mkataba wa Richmond, pengine ndiyo maana Bodi ya Tanesco ikijua utata uliogubika mchakato wa mkataba huo, ilijiepusha na mipango ya kutaka kuinunua Dowans kwa sababu ya vikwazo vya kisheria.

La kushangaza ni kwamba eti bodi baada ya kutoa maelekezo yake kwa menejimenti ya Tanesco ambayo yamepuuzwa, inafanya kampeni za chini chini ili muda wa Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo ukiisha baadaye mwaka huu, usiongezwe!

Yaani bodi imekwama kiasi kwamba haiwezi kumuwajibisha Mkurugenzi huyo au walau kuandikia mamlaka ya uteuzi wake kwamba kiongozi huyo amekiuka maelekezo yao na kwa maana hiyo aondolewe.

Bodi ya Tanesco imekuwa kama boya tu, haina nguvu wala uwezo wa kumfanya lolote Mkurugenzi Mtendaji hata pale anapoipuuza wazi wazi.

Tunajiuliza hivi Bodi ya Tanesco ina nguvu gani basi kwa ajili ya uendeshaji wa shirika hili pekee la kuzalisha nishati ya umeme nchini?

Kama Bodi haiwezi hata kumkemea Mkurugenzi Mtendaji hata pale anapoipuuza, ina sababu gani basi ya kuendelea kuwapo madarakani? Inalinda maslahi ya nani?

Sisi tunafikiri Bodi ya Tanesco kama imeshindwa kukata pembe za Dk. Rashid ina moja tu la kufanya, kujiuzulu mara moja kama ishara ya kulinda heshima yao, lakini la pili, kuwasilisha ujumbe kwa umma kwamba hawakubaliani na vitendo vya kuvunjwa kwa sheria kanuni na taratibu.

Kama Bodi haitaki kujiuzulu, ni lazima wahakikishe Dk. Rashid anajiuzulu mwenyewe ili kulinda heshima yao.

Kama haya hayatatokea, tunashawishika kusema Bodi hii haina kazi Tanesco na ni vema tu ikajiondoa yenyewe.

  • SOURCE: Nipashe

No comments: